Abstract:
Mashairi ruwaza ni dhana tunayotumia kurejela mashairi ya ‘kimaajabu’ katika taaluma ya ushairi wa Kiswahili. Mashairi haya yamekuwepo tangu miaka ya elfu mbili, hasa katika diwani za Kithaka wa Mberia. Yakilinganishwa na mashairi ya kawaida, mashairi ruwaza yanadhihirisha uchangamano mkubwa katika uwasilishaji maudhui na ufumbuaji wa maana. Hii ni kwa sababu yanatumia vipengele kama vile picha zinazoruwazwa kwa upekee wa maneno, taipografia na sitiari muono kinyume na mashairi ya kawaida yanayotumia maneno pekee na sitiari za kiisimu. Vipengele hivi vinatatiza ufasiri na welewa wa maana ya shairi ruwaza. Hivyo, kazi hii inanuia kuyajadili kwa undani huku tukichanganua mashairi teule ambayo yanapatikana katika diwani za kimapinduzi. Lengo la uchanganuzi huu ni kutajirisha stadi za usomaji na ufasiri wa mashairi ruwaza miongoni mwa wanafunzi na walimu wa ushairi wa Kiswahili. Kazi hii inalenga kujadili namna au mbinu za kufasiri sitiari muono katika mashairi haya.